Dar es Salaam. Tamko la Rais wa Kenya, William Ruto, la kuzuia usafirishaji wa malighafi bila kuchakatwa limefungua upya mjadala kuhusu nani anayenufaika zaidi na utajiri wa Afrika.
Ruto amesema madini kama magadi soda, dhahabu na lithium yanapaswa kuongezewa thamani nchini ili kuongeza ajira, mapato ya Serikali, utaalamu na fursa za biashara.
Kauli hiyo imekuja wakati Serikali yake ikisitisha shughuli za kampuni ya India, Tata Chemicals, katika eneo la Magadi, Kajiado, ikisema mfumo uliokuwepo uliwaacha wenyeji wakipata sehemu ndogo ya thamani ya rasilimali.
'Kampuni za kemikali zitaundwa hapa Kenya, zitaajiri wafanyakazi wa Kenya na kutumia rasilimali za Kenya,' amesema Ruto.
Hoja hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu Afrika, ambako sehemu kubwa ya madini, mafuta, gesi na mazao husafirishwa yakiwa ghafi, huku bidhaa zinazotokana na malighafi hizo zikirudi zikiwa na thamani kubwa zaidi.
Tanzania chini ya Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli ilipiga marufuku usafirishaji wa makinikia mwaka 2017 na kubadili mfumo wa sheria na mikataba ya madini. Hata hivyo, hatua hiyo ilisababisha mivutano ya kisheria na kampuni za madini na kufikishwa katika usuluhishi wa kimataifa.
Zimbabwe nayo ilipiga marufuku usafirishaji wa lithium ghafi mwaka 2022 na baadaye kupanua hatua hiyo hadi madini ghafi kwa ujumla mwaka 2026.
Namibia pia imepiga marufuku usafirishaji wa baadhi ya madini muhimu ambayo hayajachakatwa, ikiwamo lithium, cobalt, manganese, graphite na rare earths.
Wataalamu wanaonya kuwa nia ya kisiasa pekee haitoshi, kwani nchi zinahitaji teknolojia, umeme wa uhakika, miundombinu, sera na taasisi imara ili kuongeza thamani ya malighafi ndani ya nchi.
Mtaalamu wa diplomasia na utawala bora, Denis Konga, amesema ulinzi wa rasilimali unahitaji utashi wa kisiasa na umoja wa nchi za Afrika.
'Viongozi wengi hawaulizi Afrika tunapata nini katika rasilimali za Afrika. Kila mmoja anaangalia kwake tu,' amesema.
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Haji Semboja, amesema suala hilo haliwezi kuangaliwa kwa uzalendo pekee, kwa kuwa teknolojia, soko, sera na uwezo wa taasisi huamua kama malighafi inaweza kuchakatwa ndani.
'Teknolojia ya ndani ndiyo inaamua kama unaweza kuchakata na kuuza nje au unatakiwa kuuza malighafi,' amesema.
Mtaalamu wa Kenya, Mark Echakara, amesema Kenya ina uwezo wa kuchakata malighafi, lakini bei kubwa ya umeme ni kikwazo. Hivyo, utekelezaji wa mpango wa Ruto utahitaji uwekezaji zaidi katika umeme, miundombinu na teknolojia.
(0)Comments