Deo Ndejembi; Cheo kikubwa, hatima ngumu

Deo Ndejembi; Cheo kikubwa, hatima ngumu
View on original source
Category: Politics
Share
Archive
Like
Ni heshima kubwa kupata nafasi ya uongozi wa nchi katika umri mdogo. Ni mtihani mkubwa kulazimika kustaafu katika umri mdogo. Tunajadili hatima ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi. Julai 12, 2026, Ndejembi alitimiza umri wa miaka 43. Agosti 29, 2026, yaani wiki mbili (siku 14), tangu atimize umri wa miaka 43, alikula kiapo kuwa Makamu wa Rais. Cheo ambacho kinamfanya awe msaidizi namba moja wa Rais Samia Suluhu Hassan. Septemba 7, 2026, Ndejembi alisoma tangazo la kifo cha mwenzi wa Rais Samia, Hafidh Ameir Hassan. Kwa kupitia maelekezo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 37(3)(a), haikuhitaji utambulisho kwamba Ndejembi ndiye ameshikilia madaraka ya urais wa nchi. Katiba ya Tanzania, pamoja na usaidizi kwa rais, pia utekelezaji wa majukumu kwenye ofisi yake, vilevile inamweka makamu wa rais kwenye nafasi ya kuwa rais wa akiba. Yaani, muda wowote rais anapokuwa na udhuru wa kikatiba au anapoacha kiti wazi, makamu wa rais anashika usukani wa dola. Utaielewa hoja hii vema unaposoma Katiba ibara ya 37(5), kwamba kiti cha rais kikiwa wazi kwa sababu yoyote ile ambayo imeainishwa, nchi hairudi kwenye uchaguzi, badala yake makamu wa rais anakula kiapo na kuongoza nchi na serikali kwa muda uliobaki kukamilisha muhula. Taifa litakapofanya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2030, kama hakutakuwa na dharura yoyote katikati, maana yake Ndejembi atakuwa na umri wa miaka 47. Kama sura yake haitakuwa kwenye karatasi ya kupigia kura ama kwa nafasi ya urais, au makamu wa rais, maana yake atakuwa kwenye njiapanda ya hatima. Ataamua kustaafu akiwa na umri wa miaka 47? Ataamua kugombea ubunge? Katiba ya Tanzania haimzuii mtu aliyeshika madaraka ya makamu wa rais kuwa mbunge, endapo ataondoka kwenye nafasi hiyo. Isipokuwa, Katiba ibara ya 47(7), imekataza makamu wa rais anapokuwa ofisini, wakati huohuo kuwa mbunge au waziri mkuu. Maana yake, Ndejembi kwa umri wa miaka 47, anaweza kugombea ubunge na akishinda, ikiwa chama chake kitakuwa na wabunge wengi, inawezekana pia akawa waziri mkuu. Swali ni moja tu; kwa ngazi alizopanda, atakubali kushuka na kugombea ubunge? Haitakuwa ajabu Ndejembi kuwa mbunge baada ya kuachia madaraka ya urais. John Samuel Malecela na Cleopa David Msuya, kwa nyakati tofauti walihudumia nchi katika cheo cha makamu wa kwanza wa rais, kisha wakaendelea na ubunge wa kuchaguliwa. Ndejembi kuwa mbunge baada ya umakamu wa rais, hatakuwa wa kwanza. Tofauti ni moja, Msuya na Malecela walishika madaraka ya makamu wa kwanza wa rais kipindi cha chama kimoja. Ilikuwa kabla ya sharti la Katiba, ibara ya 47(7), kwamba makamu wa rais hatakiwi wakati huohuo awe mbunge au waziri mkuu. Msuya na Malecela, walikuwa wabunge na mawaziri wakuu, kipindi wakihudumia taifa kama makamu wa kwanza wa rais. Kwa mazingira ya sasa, Ndejembi ataweza? Chama cha Mapinduzi (CCM), kitakubali Ndejembi astaafu akiwa na umri wa miaka 47? Swali hili linakaribisha fikra za umuhimu wa kumfikiria kama mgombea urais ajaye baada ya muhula wa sasa wa Rais Samia. Kwa mujibu wa Katiba, ibara ya 40(4), Rais Samia hataruhusiwa kugombea tena, hivyo atafika kikomo chake Novemba 2030. Je, CCM wataamua kumtumia Ndejembi kwenye chama? Ama katibu mkuu au makamu mwenyekiti? Hili pia halitakuwa ajabu, maana Malecela alikuwa makamu mwenyekiti CCM, Tanzania Bara, mwaka 1997 mpaka 2007, wakati alitoka kuwa makamu wa rais na waziri mkuu. Dk Asha-Rose Migiro ni Katibu Mkuu CCM kwa sasa, wakati alishakuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ni tafakuri ya hatima ya Ndejembi kwa kuitazama kesho yake baada ya cheo chake cha sasa kufika ukingoni miaka minne ijayo. Atakuwa bado na umri mzuri wa kuendelea kulitumikia taifa. Atatakiwa kuamua kustaafu na nguvu zake, au kufanya uamuzi wa kurejea bungeni, ambao wengi wataona anajishusha hadhi? Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika alipokuwa na umri wa miaka 39. Akawa Rais wa Tanganyika akiwa na umri wa miaka 40. Hata hivyo, Mwalimu alikaa ofisini miaka 24. Alistaafu urais akiwa na umri wa miaka 63, akaachia uenyekiti wa CCM alipokuwa na umri wa miaka 68. Mfano wa Mwalimu Nyerere ni kumtangulia yule ambaye atataka kusema umri wa Ndejembi wakati anaapa kuwa makamu wa rais ni mkubwa kuliko wa Mwalimu aliposhika madaraka ya Waziri Mkuu na Rais wa Tanganyika. Hoja si umri wa sasa, bali hatima yake pale atakapotakiwa kustaafu akiwa bado na umri wenye nguvu na ari ya utumishi wa umma. Je, Ndejembi atachagua kuwa mfanyabiashara? Haitakuwa ajabu, aliyekuwa Waziri Mkuu wa UK, Tony Blair, baada ya kutumikia nafasi hiyo kwa miaka 10 (mwaka 1997 – 2007), alianzisha kampuni ya kibiashara inayoitwa Tony Blair Associates, ambayo ilijikita katika kutoa ushauri wa kiuchumi kwa serikali mbalimbali duniani, vilevile mashirika makubwa ya kibiashara. Tony Blair Associates ilianzishwa mwaka 2009. Januari 2008, Shirika la Bima la Uswis, Zurich Insurance Group, lilimwajiri Blair kama mshauri wa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO). Ni upanuzi wa muktadha kwamba inawezekana kustaafu siasa na utumishi wa umma na kushika uelekeo mwingine wa kimaisha na kufanikiwa. Mradi umri unadai. Marekani, makamu wa rais mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea kwenye nchi hiyo ni John Breckinridge. Alishika madaraka akiwa na umri wa miaka 36, na kuondoka ofisini alipokuwa na umri wa miaka 40. Baadaye alijikita kwenye taaluma yake ya sheria pamoja na biashara mbalimbali, ikiwemo za ujenzi na viwanda. Ndejembi ni msomi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa, je, akichagua kustaafu ataingia chuo kufundisha au ataanzisha taasisi isiyo ya kiserikali ili kuifaa jamii? Njia hizo mbili, ndizo wastaafu wengi huzishika. Ni tafakuri ya nia njema kwa ajili ya kesho ya Ndejembi.

(0)Comments

 

A note on cookies

Newshunt uses essential cookies to keep you signed in and to remember your language and country, so the site works the way you expect. With your permission, we'd also like to use analytics cookies to understand how people use Newshunt and improve it over time.

Accepting only affects analytics. To learn more, view our Privacy Policy or Terms & Conditions.