Wastaafu wanaosimama upande wa haki tuwalinde kama mboni ya jicho

Wastaafu wanaosimama upande wa haki tuwalinde kama mboni ya jicho
View on original source
Category: Politics
Share
Archive
Like
Wastaafu wanaosimama upande wa haki tuwalinde kama mboni ya jicho Kwa muda mrefu, kumekuwepo na kauli mbiu "Wazee ni Hazina" ikimaanisha watu wenye umri mkubwa kufikia uzee ni rasilimali kubwa ya thamani katika jamii kutokana na busara, uzoefu, na maarifa waliyonayo, lakini ghafla tunaaminishwa ni wasaliti. Utamaduni huu,mpya uliasisiwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Pombe Magufuli Ikulu ya Dar es Salaam, Septemba 11,2017 aliposema wapo viongozi wastaafu ambao wanawashwa washwa kwa kukosoa uongozi wake. Alitoa kauli hii ambayo inaonekana kuwaambukiza kizazi cha sasa cha baadhi ya viongozi wa kisiasa wasiopenda kukosolewa, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis. Katika hotuba yake, Magufuli alikuwa akiwasifia majaji wastaafu kwa utulivu na uadilifu wao na kusema:-"Bahati nzuri majaji hawa ni waadilifu sana...Ukiangalia wastaafu wa maeneo mengine hawachoki kusema, wanawashwawashwa'. Ingawa hakuwataja kwa majina, lakini wachambuzi waliona aliwalenga Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na Benjamini Mkapa kwa sababu ni Mkapa ndiye alimwambia waziwazi isiitwe 'Serikali ya Magufuli', bali inayoongozwa na CCM. Mkapa aliona hatari ya kutengeneza kiongozi mwenye nguvu badala ya taasisi yenye nguvu. Duniani kote ukiruhusu hili unakwenda kutengeneza udikteta. Kwa siku za karibuni, Waziri mkuu mstaafu na Makamu wa kwanza wa Rais, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa UN–HABITAT, Profesa Anna Tibaijuka, wamekuwa wanatoa ushauri kuliponya Taifa. Profesa Tibaijuka ni mtaalamu wa uchumi wa kilimo, mwanasiasa kutoka CCM ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Muleba Kusini tangu mwaka 2010 hadi 2020 na aliwahi kuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi. Kwa hiyo kwa vyovyote vile huwezi kutilia shaka busara yao ya nini kifanyike hasa katika kipindi hiki taifa liko katika mtanziko mkubwa kutokana na yale yaliyotokea kabla, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29,2025. Ukiacha ghasia za Oktoba 29 zilizosababisha vifo vya zaidi ya Watanzania 518 na majeruhi 2,000, lakini kuna vuguvugu la Katiba mpya, wimbi la utekaji na kupotezwa kwa watu, kuminywa kwa demokrasia na haki za binadamu. Kwa hiyo ukimuona mzee mstaafu, aliyekula chumvi na aliyewahi kushika madaraka anakaa kimya na kuona kila kitu kiko sawa nchini ana walakini. Wazee wetu hawa ni miongoni mwa wazee wanaoeleza tumefikaje hapa tulipo na tunatokaje hapa na katika kufanya hivyo lazima waeleze wapi tulipojikwaa, hapo ndio sasa baadhi ya makada wa CCM ni wale ambao hawaambiliki. Bila kuwataja kwa majina lakini Agosti 29,2026 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa Mohamed Ali Mohamed (Kawaida), alitoa kauli inayoashiria kuwanyamazisha wazee kama Jaji Warioba na Profesa Tibaijuka. Katika kauli yake aliyoitoa akizungumzia kufukuzwa uanachama kwa Dk Emmanuel Nchimbi, Kawaida alisema sio kwamba wao (CCM) hawana cha kuwajibu wala hawana hoja za kuwaambia, wazee hao ila wanawaheshimu. 'Lakini tunaheshimu nafasi waliyoitumikia katika Taifa letu, tunaheshimu kazi walizozifanya katika nchi yetu. Kama wao walivyoachwa kufanya kazi zao wasitupangie na sisi watuache tufanye majukumu yetu,'alisema. Aliongeza kusema 'na kwa sababu tunafuata Katiba na Kanuni ya CCM, kwa hiyo hatuwezi kufuata mawazo na matakwa wanayoyataka wao', mwisho wa kunukuu. Kwa maneno rahisi UVCCM na CCM haitaki tena mawazo ya wazee hao. Kuna kada mwingine, Abdul Jaffar ambaye naye amenukuliwa akipendekeza Jaji Warioba na Profesa Tibaijuka wafukuzwe uanachama wa CCM kwa kile anachodai wanaikiuka miiko, sheria na kanuni na kukisaliti Chama cha Mapinduzi. Alidai kuwa Wazee hao walipata heshima ndani ya chama lakini wao wanaona leo wanakiona kinanuka, badala ya kurudi pamoja na kukidshauri chama na kukijenga chama, wao wanashirkiana na upinzani kukidhoofisha. Lakini inaonekana kizazi cha sasa kama kina tatizo la kumbukumbu kwani hata Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere baada ya kustaafu aliendelea kuikosoa Serikali na CCM na hakuwahi kuambiwa nyamaza au anawashwa washwa. Mathalan, wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika Mbeya, Nyerere alikosoa vikali sera ya ubinafsishaji ndio akaja na ule mfano wa kupewa chupa unaambiwa ni dhahabu na unacheka kama zuzu. Nyerere alitumia mfano huo kueleza namna mali za umma zilivyokuwa zikiuzwa kwa bei ya kutupa na ukweli ni kwamba hakuwa anapinga ubinafsishaji wote, alipinga ulivyokuwa ukifanyika bila uwazi na kunufaisha wachache. Baba wa Taifa alikosoa wazi wazi Serikali na uongozi wa CCM wakati wa utawala wa Ali Hassan Mwinyi hasa katika masuala ya namna Serikali inavyoshughulikia suala la Zanzibar kuingia OIC, hoja ya Tanganyika na ile ya serikali tatu. Nyerere alienda mbali na kuandika kitabu kinaitwa 'Viongozi wetu na Hatima ya Tanzania', na katika ukurasa wa 59 alimkosoa Mwinyi:-'Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole lakini ni kiongozi dhaifu,'mwisho wa kunukuu. Lakini Nyerere ndio alikuja na usemi kuwa 'Serikali corrupt (fisadi) haikusanyi kodi' na akasema wazi wazi kuwa 'Tanzania hivi sasa inanuka rushwa'. Kwa hiyo utamaduni huu wa wastaafu kujitokeza na kunyoosha mambo pale yanapokwenda mrama hayajaanza wakati wa Jaji Warioba na Profesa Tibaijuka, la hasha, hata mwalimu anayeheshimika sana alikosoa wazi wazi Serikali. Kustaafu kwa kiongozi yeyote wa kisiasa, iwe amehudumu serikalini au ndani ya chama hamuondolei haki ya kutoa maoni yake kama mtanzania pale ambapo anaona mambo yanakwenda mrama na kauli yake inaweza kuliponya Taifa. Hiki ndio kipindi tunahitaji busara za wastaafu kuliko chochote kile na sio busara za wazee machawa na wanaojipendekeza, hapana. Tunataka busara za viongozi wakweli ambao wanasema ukweli hata kama unauma kiasi gani. Ukisoma Ibara ya 18(1) ya Katiba ya Tanzania inasema, 'bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake…' hapa haisemi bila kuathiri Kanuni au Katiba ya CCM, bali sheria za nchi. Katiba za vyama haziwezi kuwa juu ya Katiba. Huo ndio ukweli mchungu. Lakini Ibara ya 20(1) inasema kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine. Kosa la Warioba na mwenzake ni lipi. Halafu tusijisahaulishe kuwa ahadi za mwana CCM zinasema nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote na namba 8 inasema nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko, hivyo tuwaache wazee wetu waliponye Taifa letu. Kama hatukuwahi kumchukulia hatua baba wa Taifa (Nyerere) alipokuwa anaikosoa CCM na Serikali na kama tunamuenzi na kuheshimu kauli na nadharia zake, basi tuache kuwafunga midomo wazee wenye dhamira njema kwa nchi. Wazee siku zote wana hekima na uzoefu kwa sababu wamekula chumvi nyingi (wameishi miaka mingi), wameona mengi, wamepitia magumu na mazuri hivyo ushauri wao unaweza kuliokoa taifa lisiendelee kufanya makossa. Ninatamani akina Kikwete, Mizengo Pinda, Mzee John Malecela, Pius Msekwa, Frederick Sumaye na viongozi wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya CCM na serikalini, wajitokeze kuliokoa Taifa. Busara zao zinahitajika sana. Siamini kama hawajui nini kilitokea Oktoba 29,2025 na chimbuko lake. Kwa hiyo CCM isiwatishe wazee wanaotoa ushauri kulisaidia taifa letu. Kuwapa majina ni kuwakosea adabu viongozi wetu hawa tunaowaheshimu sana. Ndio maana nimetangulia kusema wastaafu ambao wamekataa kuwa chawa na kutanguliza masilahi mapana ya Taifa letu tuwalinde kama mboni ya jicho. Kwa sababu unafiki na kujipendekeza kwa masilahi binafsi kutaliangamiza Taifa letu. Daniel Mjema ni mwandishi wa habari. Ni mchambuzi wa masuala ya siasa, utawala bora na Haki za Binadamu. Anapatikana kwenye namba 065660090

(0)Comments

 

A note on cookies

Newshunt uses essential cookies to keep you signed in and to remember your language and country, so the site works the way you expect. With your permission, we'd also like to use analytics cookies to understand how people use Newshunt and improve it over time.

Accepting only affects analytics. To learn more, view our Privacy Policy or Terms & Conditions.