(PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) Wamekubaliana Kujenga Ushirikiano wa Kimkakati Unaolenga Kupanua Wigo wa Utoaji wa Elimu Kwa Umma

(PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) Wamekubaliana Kujenga Ushirikiano wa Kimkakati Unaolenga Kupanua Wigo wa Utoaji wa Elimu Kwa Umma
View on original source
Category: Entertainment
Share
Archive
Like
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) wamekubaliana kujenga ushirikiano wa kimkakati unaolenga kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu hifadhi ya jamii, mifumo ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo. Hatua hiyo imefuatia ziara rasmi ya timu ya maofisa wa PSSSF katika Makao Makuu ya TBN yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ambako ilifanya mazungumzo na viongozi wa mtandao huo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa habari, uelimishaji wa umma na usambazaji wa taarifa sahihi kupitia majukwaa ya kidijitali. Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo wenye wanachama zaidi ya 200 nchi nzima na Diaspora, upo tayari kutumia uwezo, uzoefu na wigo wa majukwaa ya wanachama wake kutoa elimu sahihi kuhusu shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na PSSSF. Hata hivyo, Msimbe alisisitiza umuhimu wa wanachama wa TBN kupatiwa mafunzo ya kina kuhusu shughuli, huduma na uendeshaji wa mfuko huo, ili waweze kuielimisha jamii kwa usahihi na ufanisi zaidi. Alisema ushirikiano huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo waliopo katika maeneo ambayo taarifa kuhusu hifadhi ya jamii na mifumo ya pensheni hazijawafikia kwa kiwango cha kutosha. Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya jitihada za mfuko kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii. Njaidi aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi, mapendekezo na hoja zote zilizowasilishwa katika mkutano huo zitafanyiwa kazi. Alisema dhamira ya PSSSF ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni, hifadhi ya jamii pamoja na uwekezaji unaofanywa na mfuko kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla. Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una historia kubwa katika maendeleo ya habari za kidijitali nchini na unajivunia kuwa na wanachama wenye weledi, uzoefu na uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali. Michuzi alisema TBN ilianzishwa kwa dhamira ya kuhakikisha Tanzania inasomeka vizuri katika medani za kidijitali, kwa kusambaza taarifa sahihi zinazochochea maendeleo na kusaidia kutanua gurudumu la uchumi wa Taifa. 'TBN ipo tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka kupitia majukwaa ya kidijitali,' alisema Michuzi. Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo upo tayari kutumia waandishi wake mahiri na majukwaa mbalimbali ya wanachama wake kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, zenye kuaminika na zitakazowawezesha kuelewa vyema haki, wajibu na fursa zinazopatikana kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii. Alisema ushirikiano wa PSSSF na TBN unaweza kuwa daraja muhimu la kuunganisha taasisi hiyo na wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho majukwaa ya kidijitali yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya habari na maarifa. Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo. Kwa upande wa TBN, mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi.

(0)Comments

 

A note on cookies

Newshunt uses essential cookies to keep you signed in and to remember your language and country, so the site works the way you expect. With your permission, we'd also like to use analytics cookies to understand how people use Newshunt and improve it over time.

Accepting only affects analytics. To learn more, view our Privacy Policy or Terms & Conditions.