Dar es Salaam. Sera ya Chama cha ACT-Wazalendo ya 'Zanzibar yenye mamlaka kamili' imeibua mgongano wa hoja, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira kuhoji iwapo dhana hiyo inaashiria Zanzibar kuwa Taifa huru na huo kuwa mwisho wa Muungano.
Wasira amesema madai ya mamlaka kamili kwa Zanzibar yanahitaji ufafanuzi zaidi, akitaka kufafanuliwa iwapo yanakusudia kuimarisha mamlaka yaliyopo ndani ya Muungano au yanaashiria Zanzibar kuwa na hadhi ya nchi huru.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema sera hiyo hailengi kuvunja Muungano, bali kurekebisha changamoto za kikatiba zinazozua migogoro ya mamlaka kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema chama hicho kiko tayari kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, baada ya kukamilika mchakato wa kamati ya pamoja kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM). pic.twitter.com/sg8mQeKcgV — Mwananchi Newspapers (@MwananchiNews) September 8, 2026
Kwa mujibu wa chama hicho, maboresho ya Katiba yanahitajika ili kila upande utekeleze kikamilifu mamlaka yake katika masuala yasiyo ya Muungano, huku mambo ya Muungano yakiendelea kusimamiwa kwa utaratibu uliokubaliwa.
Wakati Wasira na Othman wakiibua hoja hizo ,' wachambuzi wa siasa wanasema mjadala huo unaonyesha umuhimu wa kuwepo kwa ufafanuzi wa kikatiba na kisera kuhusu mgawanyo wa mamlaka.
Mjadala huo umeibuka leo, Jumanne, Septemba 8, 2026, wakati wa maswali na majibu ya wadau katika Mkutano wa Kitaifa wa Wadau unaolenga kutafakari hali ya kisiasa nchini, Uchaguzi Mkuu wa 2025 na mustakabali wa Taifa.
Aliposimama kuchangia mjadala huo, Wasira alielekeza swali kwa Othman, akihoji maana sera ya ACT - Wazalendo ya Zanzibar yenye mamlaka kamili, akisisitiza huwa anapata taabu kujua mamlaka ni yapi na kamili ni ipi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amehoji maana ya kauli ya 'Zanzibar yenye mamlaka kamili' inayotajwa katika sera ya Chama cha ACT-Wazalendo. pic.twitter.com/K5dH1mRiw9 — Mwananchi Newspapers (@MwananchiNews) September 8, 2026
"Hivi Zanzibar ambayo ni sehemu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba, inayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwa kweli inashughulika karibu na mambo yote ya Zanzibar, isipokuwa mambo machache sana ambayo yako ndani ya muungano – ulinzi, mambo ya nje, mambo ya ndani, elimu ya juu na hali ya hewa. Sasa unaposema Zanzibar yenye mamlaka kamili sasa inakuwa sehemu ya Muungano au inakuwa sovereignty (nchi huru)," amehoji.
Wasira ameendelea kuhoji kama Zanzibar linakuwa Taifa huru huo ndio mwisho wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au inakuaje?
"Hili jambo kubwa ambalo nalo tusipolifanyia ufafanuzi linayumbisha watu na linatuletea hata sisi huku Bara mgogoro. Wenzetu kule wanasema wanataka mamlaka kamili sasa wengine kule wanasema na Tanganyika je?" amehoji.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kutasaidia kuleta utulivu wa kisiasa Zanzibar na Tanzania Bara. pic.twitter.com/Gti4mDe0Kp — Mwananchi Newspapers (@MwananchiNews) September 8, 2026
Katika hoja hiyo, amesema mamlaka kamili unazungumzia uhuru wa Zanzibar, lakini hakuna uhuru wa Tanganyika, isipokuwa uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Tukiweka katika maana ya elimu itatusaidia kujibu hoja za wale ambao wanadhani Zanzibar inapendelewa katika muungano. Wengine wanasema inaonewa wengine wanasema inapendelewa," amesema.
Akijibu hoja za Wasira, Othman amesema msingi wa dhana ya Zanzibar yenye mamlaka kamili unatokana na namna Muungano unavyotekelezwa na si suala la kuvunja Muungano.
Amesema kuna mambo yaliyoainishwa kwenye Katiba, lakini utekelezaji wake umekuwa tofauti, hali ambayo imeifanya Katiba kuwa miongoni mwa vihatarishi vya migogoro ndani ya Muungano.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismael Jusa, amesema si lazima mazungumzo ya kisiasa ya yasimamiwe na msuluhishi wa nje ili yawe na tija, akieleza kuwa uzoefu wa Zanzibar mwaka 2001 unaonyesha kuwa pande zinazohusika zinaweza kufikia mwafaka zenyewe. pic.twitter.com/dwcEMdVN3g — Mwananchi Newspapers (@MwananchiNews) September 8, 2026
Othman, ametaka maboresho ya Katiba ili Zanzibar isionekane imechukua mamlaka yasiyo yake katika masuala yasiyo ya Muungano, bali itekeleze kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
"Lakini huu ndio mfumo ulioundwa chini ya muungano. Mambo ya muungano yanapaswa kutekelezwa kwa muungano, lakini yasiyo ya muungano, Zanzibar na kila upande utakuwa na mamlaka kamili kuhusu mambo husika," amesema.
Amesema masuala yaliyokubaliwa kuwa ya Muungano yanapaswa kusimamiwa kwa utaratibu huo, huku kila upande ukiachiwa mamlaka yake katika mambo yasiyo ya Muungano bila kuingiliwa na upande mwingine.
Amesisitiza kuwa Muungano unapaswa kujengwa kwenye misingi imara ya kikatiba ili kuhimili mabadiliko ya kisiasa na kuendelea kudumu bila kutegemea uhusiano wa viongozi waliopo madarakani.
"Ikitokea leo Zanzibar inaongozwa na chama kingine muungano huu uendelee, isije ikawa vurugu. Ikitokea leo kuna chama kingine Tanzania Bara muungano uendelee isiwe vurugu.
Mimi ninavyosema kwa sasa ikitokea chama kingine itakuwa ngumu kwa muungano, kwa kuwa mambo mengi tunaendesha kwa kujuana," amesema Othman.
Akizungumzia mjadala wa vigogo hao, Mchambuzi wa siasa, Dk Baraka Mfinanga amesema kunahitajika ufafanuzi wa kikatiba na kisera ili kuondoa tafsiri zinazoweza kuibua hofu ya kuvunjika kwa Muungano au hisia za upande mmoja kunufaika zaidi.
'Mjadala huu ni muhimu kwa sababu unaenda moja kwa moja kwenye tafsiri ya mamlaka ndani ya Muungano. Wananchi wanahitaji kujua iwapo mamlaka kamili inamaanisha uhuru wa kujitawala au mabadiliko ya muundo wa Muungano,' amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amesema mchakato wa uandishi wa Katiba mpya unapaswa kuzingatia historia ya Tanzania na si kuonekana kama hatua ya kuanzisha nchi mpya. pic.twitter.com/HfyXNJlj7B — Mwananchi Newspapers (@MwananchiNews) September 8, 2026
Amesema hoja hiyo inaakisi mjadala wa muda mrefu kuhusu usawa wa mamlaka kati ya Zanzibar, Tanganyika na Serikali ya Muungano, jambo ambalo bado halijapatiwa majibu ya pamoja kisiasa.
Kwa upande wake, Said Majjid, mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, amesema mjadala huo unapaswa kutazamwa kama fursa ya kutafuta mwafaka wa kikatiba utakaoimarisha Muungano badala ya kuudhoofisha, huku ukiongeza uwajibikaji wa taasisi za pande zote mbili.
'Maelezo ya Othman yanaonyesha kuwa ACT -Wazalendo haisukumi ajenda ya kuvunja Muungano, bali inataka mfumo unaofafanua vizuri mipaka ya mamlaka kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano,' amesema.
Amesema migogoro mingi ya Muungano imekuwa ikitokana na tafsiri tofauti za Katiba na utekelezaji wa mamlaka katika mambo yasiyo ya Muungano, jambo linalohitaji majadiliano ya wazi.
Mengine waliyojadili
Mbali na majadiliano kuhusu sera ya ACT- Wazalendo, katika mjadala huo, Wasira amezungumzia siasa, akisema kwa kawaida haijanyooka na huwa inabadilika kulingana na mazingira na watu.
"Huwezi ukaichukua siasa kwa asilimia 100 kwamba hawa tunaowaita walio wengi kwamba wanakubali kwa kuwa kesho wanaweza wasikubali," amesema.
Wasira, ametumia jukwaa hilo pia kuipongeza Zanzibar kwa kusaini tamko la pamoja la kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ingawa ametilia shaka hatua ya ACT - Wazalendo kuchelewa kuingia serikalini.
Amesema wakati mwingine kizazi kipya kinapata taabu kuelewa umuhimu wa muungano, lakini wanachopaswa kuelewa ni kuwa amani, utulivu wa Zanzibar na Tanganyika vinategemeana.
"Zanzibar kulikuwa na mapinduzi, walipinduana lakini siri ya mapinduzi yale ni kwamba ASP walienda Uingereza kukubaliana ikashindikana.
Ameeleza tofauti zilizopo katika uundwaji wa SUK zinaweza kutatuliwa na Serikali hiyo ikaundwa.
Mwandishi wa habari mkongwe nchini, Salimu Mohamed Salimu amesema jitihada za kufikia mwafaka na maridhiano ya kisiasa hazipaswi kuendeshwa kwa usiri bali kwa uwazi unaowapa wananchi nafasi ya kujua na kushiriki.
Amesema mwafaka ni haki ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara, hivyo hawapaswi kufichwa kile kinachojadiliwa, huku akikosoa usiri uliotawala mazungumzo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kuwa hata vyombo vya habari vinakosa fursa ya kufuatilia mchakato huo kikamilifu.
Mkwamo wa SUK
Katika hatua nyingine, Othman amesema chama hicho kiko tayari kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa mara baada ya kamati ya pamoja kati ya ACT -Wazalendo na CCM kuanza kazi rasmi.
Amesema kamati hiyo yenye wajumbe kutoka pande zote itafuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa, ikiwemo kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ya Zanzibar.
Pia, kutaundwa Tume ya Utekelezaji itakayoshughulikia changamoto zilizobainishwa na kusimamia utekelezaji wake hadi mwaka 2029.
Othman amesema hatua hizo zinalenga kujenga mfumo imara wa kisiasa unaoweza kulinda amani, kuimarisha utawala na kukuza uchumi wa Zanzibar.
(0)Comments